JIFUNZE NAMNA YA KUANDIKA MKATABA KISHERIA UNAPOUZA AU KUNUNUA
Na Bashir Yakub
Katika shughuli zetu za kuuza na kununua ambazo tunazifanya kila siku mikataba ya maandishi ni jambo ambalo wengi tunakutana nalo. Mikataba hii iwe rasmi au isiwe rasmi suala la msingi ni kuwa huwa tunaifanya. Aidha wakati mwingine si wote wenye kuhusisha suala la mikataba ya maandishi katika makubaliano yaombalimbali na hii hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuaminiana. Kuhusu kuaminiana niseme jambo moja tu kuwa suala la mikataba ni muhimu sana hata kana mwenzako unamuamini kwa kiwango cha juu kabisa( highest degree of trust).
Nathubutu kusema kuwa hata awe mzazi wako kama kuna
jambo la msingi mmelifanya ni vema kukawapo mkataba wa maandishi.
Nasema hivi kwakuwa kwa uzoefu wangu wa mambo haya mara nyingi mgogoro
hautokani na waliouziana au kukubaliana isipokuwa mgogoro unakuja
kuanzishwa na walio nyuma ya hao.
Kwa
mfano baba anaweza kumpa mwanae kiwanja na wasifanye mkataba wowote
wa maandishi kwa kuwa wanaaminiana. Hiyo ikaenda kwa miaka kadhaa
ambapo baba akawa amefariki. Baaada ya hapo anaibuka mtu anasema mimi
ni mtoto wa marehemu kwa hiyo nahitaji kiasi kadhaa kutoka mali hii.
Hapa mgogoro si kati ya baba na mwana tena isipokuwa ni kati ya mwana na mtu mwingine. Kama huna
mkataba wowote wa maandishi mpaka kesi hii kuisha waweza kuwa
umepoteza kila kitu. Huu ni mfano tu katika kusisitiza kuwa mtu asiseme
mi na fulani tunaaminiana. Mgogoro sio lazima utokane na nyie wawili
isipokuwa walio nyuma yenu waweza kuanzisha mgogoro.
1. MADHARA YA KUTOFANYA MKATABA WA KISHERIA .
Ni vema sana kujihadhari
kwakuwa ukisikia neno mgogoro ujue kuna mambo makubwa mawili. Kwanza
gharama kubwa ni uwezekano wa kupoteza kabisa ile mali na haijalishi iwe uliinunua au ulipewa isipokuwa tu ukishakuwa na mgogoro upo katika hatari hiyo. Pia gharama ya pesa kama kuwalipa
wanasheria, gharama za uendeshaji kesi, nauli na matumizi mengineyo
ambayo hujitokeza bila hata kutarajia. Pili kuna gharama ya muda .
Hii
huhusisha kushinda mahakamani kila siku na wote mwajua mahakama
zetu zilivyo, kushinda vituo vya polisi huku shughuli zako za msingi za
kila siku zikisimama. Pia hapa kuna muda wa kusubiri hukumu ambapo
kesi yaweza kukaa mahakamani hata miaka sita . Hakika unakuwa
umesurubika(suffer) na umepoteza mambo mengi katika kushughulikia jambo
hili.
2. USHAURI.
Ushauri
wa kawaida tu kwa hili ni kuwa na utamaduni wa kuweka katika maandishi
kila makubaliano na hii iwe kwa watu wote mnayeaminiana sana au
msiyeaminiana. Fanya hili kuwa utamaduni wako kwa kuweka kila muamala
wako katika maandishi suala la kuaminiani lisiwe hoja tena kwakuwa
mgogoro hautakuwa kati yako na yeye isipokuwa unaweza kuwa kati ya mtu
wa nyuma yake na wewe au mtu wa nyuma yako na yeye. Nitatoa
mfano mwingine halisi ambapo mfano huu ni kesi ipo mahakamani hadi
leo.
Mwaka
2010 mwezi wa saba mtu mmoja alimuuzia rafiki yake gari aina ya land
cruiser akiwa anatafuta fedha kwa ajili ya safari yake ya uingereza
baada ya kupata kazi huko. Wakauziana na kwakuwa waliaminiana sana hawakuandikishana popote.
Mwaka
mmoja na nusu baadae gari hiyo ikakamatwa maeneo ya Sinza na polisi
kwasababu kuwa mwaka 2009 Disemba iliwagonga watu wawili na kuuwa mmoja
maeneo ya tabata na kukimbia. Mnunuzi alijitetea kwa urahisi tu kuwa
gari amelipata 2010 July kwa hiyo hawezi kuwa anahusika na lolote kabla
ya muda huo.
Utetezi wake ulikubaliwa
isipokuwa tu alitakiwa atihibitishe kwa kuonesha mkataba halali wa
mauziano ambao utaonesha kuwa ameanza kumiliki gari hilo
baada ya ajali. Ilikuwa vigumu kwake na hilo likamwingiza moja kwa
moja katika kesi hiyo na mpaka naandika makala haya amesota na kesi
hiyo kwa miaka minne sasa na haijajulikana inaisha lini ambapo kwa
mtazamo wa kitaalam kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana na hatia na
kwenda jela.Kwa hiyo utaona hapa kuwa kufanya maandiko ya kisheria
katika kila muamala si muhimu tu katika kudhulumiana bali pia hata
mambo mengine kama haya ambayo yanaweza kujitokeza bila kutarajia.
3. JE KILA MAANDISHI NI MKATABA.
Aidha
uandishi mzuri wa mkataba wa kisheria hupelekea mkataba wenye hadhi na
mkataba wenye hadhi ndio mkataba halali ambao hukubalika kisheria na
pia huweza kutumika kama ushahidi
endapo kuna tatizo. Yawezekana unao mkataba lakini hauna hadhi kisheria
na likijitokeza jambo mkataba wako hautakubalika. Si kila maandishi ni
mkataba isipokuwa mkataba huwa na vitu maalum vya kisheria ambavyo
huufanya kukubalika na kutambuliwa. Haya hapa ndio mambo ya msingi
ambayo hutakiwa kuwa ndani ya mkataba.
4. MKATABA MZURI HUWA NA HAYA :
( a ) Lazima
uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu na kwa
kueleweka.Mfano jina liwe Paschal Mayenge Archard. Epuka kuandika
vifupi mfano P.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake
na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina ya pande zote mbili
yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo si tu majina ya upande
mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi pia ni
muhimu majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama wako ishirini.
( b ) Katika
majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano
kama ni muuzaji au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu
ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi
mpokea zawadi viainishwe.
( c )
Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani
namba mfano 1,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni moja
tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya
mkataba ioneshwe sambamba na maelezokama fedha imelipwa yote au kiasi.
( d ) Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno kama nilivyoonesha
hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na
hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba lazima uoneshe
muda ukipita nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi
jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi mali itamrudia
mwenye nayo na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au
itahesabika kuwa mkataba umevunjika na mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia
ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.
( e ) Mashahidi
ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si
mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu.
Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo ya wahusika na pia
wataweka sahihi zao huku ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi
wa upande upi. Wakili ni mtu muhimu sana kwa wakati huu kwani wakili anaweza kuwa shahidi pekee bila kuwapo shahidi mwingine yeyote.
Wakili
anakuwa shahidi wa wote wawili na panakuwa hapahitajiki mwingine
yeyote.Pia wakili ni shahidi wa kuaminika zaidi na anaaminiwa na kila
mamlaka ikiwemo mahakama na hivyo uwepo wake katika mkataba ni ulinzi
tosha kwa mkataba wako.
( f ) Mali inayouzwa
au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema. Kama ni kiwanja au
nyumba ielezwe mtaa, kata, tarafa kitongoji,mkoa,plot namba kama ipo,
urefu, upana, ikiwezekana jirani wa kushoto na kulia.au magharibi,
mashariki, na kama ni gari, pikipiki maelezo yote yaliyo kwenye kadi
yaingie katika mkataba ili kutambua kwa undani mali yenyewe.
( g ) Anuani za muuzaji au mnunuzi ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la namba ya simu ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.
( h ) Picha ndogo yenye kuonesha taswira ya mtu kwa ukamilifu (passport size) ni muhimu sana na ibandikwe mbele ya jina la mtu. Si muhimu sana kwa mashahidi lakini kwa wahusika wenyewe ni muhimu sana.
( I ) Alama ya dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana.
Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au
kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele
ya kila jina. Hii pia si lazima kwa mashahidi.
( j ) Kama ni kiwanja au nyumba ni muhimu mkataba uoneshe kama kimelipiwa kodi ya ardhi ( Land rent) na kama hakijalipiwa mkataba ueleze nani atalipa kodi hiyo kati ya anayenunua au anayeuza.
( k ) Pia
ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana
na mkataba huo nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea
kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka ndio
itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo mkataba uweke wajibu kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano mnunuzi iwapo mali aliyomuuzia
itaonekana kuwa na mgogoro mbeleni mfano muuzaji atampa ushirikiano
mnunuzi endapo kutatokea mgogoro wowote kuhusiana na mauziano haya.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NDIYE MWANZILISHI NA MKURUGENZI WA BLOG HII.
0784482959,
0714047241,
bashiryakub@ymail.com
JIFUNZE NAMNA YA KUANDIKA MKATABA KISHERIA UNAPOUZA AU KUNUNUA
Reviewed by crispaseve
on
23:23
Rating:
Post a Comment