MNUNUZI WA GARI JIHADHARI NA UTAPELI HUU WA KIMKATABA .
Na Bashir Yakub
1. KUTAPELIWA
KATIKA UNUNUZI WA GARI.
Ununuzi wa magari sawa na
biashara nyingine yoyote unahitaji umakini. Lakini ununuzi wa gari unahitaji umakini mkubwa zaidi pengine
kuliko mali nyingine yoyote inayohamishika
kwa sasa. Hii ni kutokana na kukua kwa biashara ya bidhaa hiyo kulikoleteleza
kujipenyeza kwa matapeli hasa mijini.
Utapeli wa magari ni mkubwa kuliko watu
wanavyofikiria na idadi ya wanaotapeliwa kwa siku inaelekea kulingana na idadi
ya magari yanayouzwa kwa siku. Si rahisi
kulijua hili kama hufuatilii mambo haya. Uzuri au ubaya, wanaofanya matukio
haya ni walewale. Nafasi kubwa wanayotumia ni ulaghai wa kimkataba na wanatumia
mapungufu ya mkataba kumtapeli mtu halafu wanaendelea kuwapo na huna la kufanya
sababu mkataba wako una mapungufu ambayo
uzito wake kisheria ni kama huna mkataba.
Aliyekutapeli atakuwapo na hutakuwa na la kufanya kwasababu ya msemo wa kisheria
usemao “Buyer Be Aware”(Mnunuzi kuwa Makini). Umakini wako ni katika kufanya
mkataba utakaolinda manunuzi yako. Lau ukifanya kosa sheria imeshasema hivyo imemaliza.
2. MKATABA
SALAMA WA KUNUNULIA GARI LAKO HAKIKISHA UNA TAARIFA
HIZI.
( a ) Lazima
uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu na kwa
kueleweka.Mfano jina liwe Aloys Mayenge Archard. Epuka kuandika vifupi
mfano A.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na
majina matatu kamili. Pia majina ya pande zote mbili yaani muuzaji na
mnunuzi yatokee hivyohiyvo si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana
mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi pia ni muhimu majina
matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama wako ishirini.
( b ) Katika
majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni
muuzaji au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni
mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi mpokea zawadi
viainishwe.
( c )
Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba
mfano 10,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni kumi tu).Ni muhimu
yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe
sambamba na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.
( d ) Kama
kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa
maneno kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki
nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa
utapita. Mkataba lazima uoneshe muda ukipita nini kifanyike mfano
ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa
basi gari litamrudia muuzaji na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya
muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika na mnunuzi
atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.
( e ) Mashahidi
ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya.
Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika
majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo ya wahusika na pia
wataweka sahihi zao huku ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa
upande upi.
( f ) Gari iliyouzwa
au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema.Mfano chasis No, aina ya
bodi,watengenezaji,rangi,namba kama imesajiliwa,uwezo wa injini,aina ya mafuta
inayotumia,mwaka iliyotengenezwa n.k.
( g )Mkataba ni lazima ueleze gari imeingia nchini ikitokea
wapi kama ni Japan,Dubai n.k.
( h ) Anuani
za muuzaji au mnunuzi ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la
namba ya simu ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa
wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.
( I ) Alama
ya dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na
alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye
kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Na hapa ndipo
wanapokamatiwa matapeli walio wengi. Hatua hii pia si lazima kwa mashahidi.
( j ) Lazima
mkataba ueleze kama gari imelipiwa leseni ya barabarani( road licence), bima, na kama ililipa
ushuru wote muhimu unaotakiwa wakati wa kuingia nchini.Kama haijalipiwa baadhi
au vyote mkataba ueleze na deni liainishwe.
( k ) Ni
muhimu pia mkataba uoneshe iwapo gari lina
tatizo lolote la kiufundi(machenical problem) kama hapana basi isemwe nini
kifanyike kama muda mfupi baada ya manunuzi litagundulika tatizo ambalo muuzaji
hakulisema.
( L ) Pia ni
muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mauzo ya
gari nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba
huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka ndio itahusika na utatuzi wa
mgogoro. Sambamba na hilo mkataba uweke wajibu kwa muuzaji
kuwa tayari kumpa ushirikiano mnunuzi iwapo gari alilomuuzia
litakuwa na mgogoro kuhusu wizi,ushuru,mkopo, au mgogoro wowote unaotokana na
mkataba wa mauziano hayo.
( M ) Aidha
kipengele kinachomtaka muuzaji kurejesha fedha yote au sehemu yake iwapo jambo
fulani litatokea pia chaweza kuwekwa.
3.TUSIPENDE KUFANYA MAMBO KIENYEJI.
Muda wa kufanya mambo kienyeji umekwisha. Dunia imebadilika sana
lazima watu walikubali hili. Ieleweke kuwa kufanya mambo kienyeji kuna gharama
zake kubwa tu. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kuua mtu jana.
Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kushiriki katika uhalifu mkubwa wiki iliyopita.Haya yote
utayajibu vipi na yataisha lini. Unaweza kuuziwa gari ambayo haikulipa ushuru
kwakuwa imesajiliwa kama inasafirishwa(
IN TRANSIT, IT) si ya hapa nchini,
vipi utamaliza kesi na mzigo wa mamilioni ya deni la ushuru. Jihadhari ndugu
epuka kufanya mambo kienyeji.
.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA
NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA SERIKALI LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA
JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. PIA NI MKURUGENZI NA MWANZILISHI WA BLOG HII
0784482959,
0714047241,
bashiryakub@ymail.com
MNUNUZI WA GARI JIHADHARI NA UTAPELI HUU WA KIMKATABA .
Reviewed by crispaseve
on
23:30
Rating:
Post a Comment