DENGUE YAINGIA ZANZIBAR, WATATU WAGUNDULIKA

Baadhi ya
waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Afya Zanzibr
Juma Duni Haji kufuatia kugundulika kwa wagonjwa watatu wa Dengue.
Watu
watatu wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibar baada
ya kushukiwa kuwa na maradhi ya homa ya Dengue inayosababishwa na mbu
aina ya “Aedes”.
Ugonjwa huo tayari umeingia jijini Dar es Salaam na kuathiri watu zaidi ya 400 huku wengine wakiripotiwa kufariki.
Akizungumza
na waandishi wa habari visiwani hapa, Waziri wa Afya, Juma Duni Haji,
alisema, wagonjwa hao wametokea katika maeneo ya vijiji vya Kama na
Mwera.
Alisema,
tokea wagonjwa hao wabainike, uongozi wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja
umeamua kuchukua vipimo kwa ajili ya kuvifanyia uchunguzi zaidi, ikiwa
ni hatua ya kuweza kupata uthibitisho wa wagonjwa hao kama wanaugua homa
hiyo.
“Serikali
kupitia Wizara ya Afya imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo
kuchukua vipimo (Sample) ili kuchunguza kuwepo kwa virusi hivyo na
kufuatilia sehemu walikotoka wagonjwa ili kutathmini hali halisi ya
mazingira”, alisema Waziri huyo.
Waziri
Duni, alisema, wanalazimika kuchukua hatua hiyo kwa vile maradhi hayo ni
mara ya kwanza kujitokeza hapa Zanzibar, hivyo ni vyema wananchi
wakaona umuhimu wa kusafisha mazingira yanayowazunguka.
Aidha,
alifahamisha kuwa hadi sasa hakuna tiba maalum ya ugonjwa huo, na kwamba
mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana kama vile homa,
kupungukiwa na maji au damu huku akisisitiza hakuna chanjo kwa ajili ya
kinga.
Waziri
Duni, alisema katika kukabiliana na ugonjwa huo, serikali hivi sasa,
inawasiliana na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili yaweze kuwasaidia
katika kuleta vifaa vya uuguzi kwa wagonjwa watakaopatwa na tatizo hilo.
Aliyataja mashirika ambayo wameanza kuwasiliana nayo ni pamoja na WHO, NIMR na Wizara ya Afya Tanzania Bara.
Waziri wa
Afya Zanzibar Juma Duni Haji akizungumza na waandishi wa habari juu ya
hofu ya kuwepo kwa wagonjwa watatu wanaoshakiwa kuwa na dalili za
ugonjwa wa Dengue.
Alizitaja
dalili za ugonjwa huo ni homa ya hafla,mwili kuchoka, kuumwa na viungo,
kuvimba tenzi na kupatwa na haraha (Vipele), kuumwa na kichwa ambapo
dalili zake huanza kujitokeza kuanzia kati ya siku tatu na 14 tangu mtu
alipoambukizwa.
“Dalili
za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria na homa ya
mafua, hivyo nawaomba wananchi kuwa waangalifu hasa wakati wanapopata
homa ambazo zinafanana na malaria kukimbilia vituo vya afya,” alisema.
Hata
hivyo, alifahamisha kuwa kuna aina tofauti za ugonjwa huo, ikiwemo
(Dengue Fever) ambapo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ghafla,
kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.
Dk. Salma
Masauni Yussuf, ambae ni Mkuu wa Kitengo cha kuzuia na kudhibiti
maradhi Zanzibar, aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja ili
kuhakikisha hali inakuwa nzuri hapa nchini huku akiwanasahi kusafisha
mazingira hasa katika kipindi hichi cha mvua za masika zinazoendelea.
DENGUE YAINGIA ZANZIBAR, WATATU WAGUNDULIKA
Reviewed by crispaseve
on
02:27
Rating:
Post a Comment