Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
--
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la
upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa
chini.
Ametoa agizo hilo juzi (Jumamosi, Mei 24, 2014) wakati akizungumza na viongozi na
watendaji wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo,
Ikulu ndogo, mjini Sumbawanga.
Waziri Mkuu amewasili
mkoani Rukwa jana jioni akitokea Dodoma ambapo atamwakilisha Rais Jakaya
Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali
wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa itakayofanyika leo
(Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini
Sumbawanga.
Akifafanua kuhusu tatizo
la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama mkoa ili muweze
kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati kwa watoto
wetu wa shule za msingi”.
“Lazima mje na mpango
maalum… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni hizo mbao
zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende kutengeneza madawati
na yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda shule fulani, na
utaratibu uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
Alisema utaratibu huo
unaweza kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwa uhakika zaidi kwani
hata Halmashauri zinapoamua kupiga mnada mbao zilizokamatwa, fedha
inayopatikana huwa haiendi kutengeneza madawati.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka idara za elimu za mkoa wa Rukwa, Halmashauri tatu za wilaya za
mkoa huo ambazo ni Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Vijijini zinakabiliwa na
upungufu wa madawati 33,799, wakati mahitaji ya madawati ni 62,118 na
yaliyopo ni 28,319. Manispaa ya Sumbawanga ilisema ina upungufu wa
madawati 675 bila kutaja yaliyopo ni mangapi wala mahitaji yake ni kiasi
gani.
Akizindua Wiki ya Elimu
Kitaifa mjini Dodoma Mei 3, mwaka huu, Waziri Mkuu aliitaka Ofisi ya
Waziri Mkuu – TAMISEMI ambayo inasimamia sekta ya elimu iandae utaratibu
wa kuzibana Halmashauri ziwe za mjini au vijijini kwani zote zina uwezo
wa kupunguza tatizo hilo kulingana na fursa zilizonazo. “Nasisitiza
jambo hili liwe ni ajenda ya kudumu,” alisema Waziri Mkuu.
Mei 14, 2014, wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) jijini Tanga, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti wa
Halmashauri kuhakikisha wanamaliza tatizo la madawati kwani nyenzo
wanazo kupitia Halmashauri wanazoziongoza.
Mapema, akiwasilisha
taarifa ya Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Stella Manyanya
alisema mkoa huo kupitia kamati za shule na uongozi wa kata umeweka
mkakati wa kutatua tatizo la madawati kama njia mojawapo ya kuboresha
taaluma katika mpango wa Matokeo Makubwa na ya Haraka (BRN).
Akizungumzia kuhusu hali
ya miundombinu katika Mkoa huo, Eng. Manyanya alisema kazi za ujenzi wa
barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami unaendelea sasa baada ya
msimu wa mvua kumalizika na baadhi ya wakandarasi kupatiwa fedha na
Serikali.
Kuhusu usanifu wa Daraja
la Mto Momba lililoko mpakani mwa mikoa ya Rukwa na Mbeya, Eng.
Manyanya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo imesimama kutokana na
kina cha maji kupanda licha ya kuwa ilipaswa kukamilika tangu Machi
mwaka huu.
“Usanifu ulitarajiwa
kukamilika Machi 2014, lakini kutokana na kina cha maji kupanda,
uchunguzi wa matabaka ya udongo chini ya maji umeahirishwa mpaka maji
yatakapopungua,” alisema.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa
Mkoa alisema wanatarajia kazi ya usanifu na uandaaji wa nyaraka za
zabuni utakamilika mwezi Mei mwishoni na baada ya hapo zabuni kwa ajili
ya ujenzi wa daraja hilo itatangazwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MEI 25, 2014
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.
Reviewed by crispaseve
on
02:24
Rating:
Post a Comment