ATCL: Utawala wa Rais Kikwete umetulindia hadhi yetu
SHIRIKA la ndege la taifa (ATCL) limeupongeza utawala
wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete huku likibainisha kuwa licha ya
changamoto zilizo likabili shirika hilo katika kipindi cha awamu hiyo bado
limefanikiwa kulinda hadhi yake sambamba na kuibua mipango inayolenga kuliibua
upya shirika hilo.
Akizungumza mbele ya
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na utendaji wa shirika hilo katika kipindi hicho
cha awamu ya nne, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bw. Johnson
Mfinanga aliitaja baadhi ya mikakati iliyoundwa juu ya msingi wa serikali ya
awamu ya nne katika kuboresha zaidi huduma za shirika hilo.
“Ni katika kipindi hiki cha awamu ya nne chini
ya Rais Kikwete ndio tuliweza kuanzisha
safari zetu za kwenda visiwa vya Comoro na tumekuwa tukizidi kuongeza safari
zetu zaidi kuelekea huko kwa kuwa tumebaini uamuzi huu umekuwa na tija kwa
wananchi wa mataifa haya mawili,’’ alibainisha Bw. Mfinanga ambaye shirika lake
kwa sasa limeongeza idadi ya safari zake kuelekea visiwa hivyo kutoka mara tano hadi kufikia mara saba kwa
wiki.
Kwa sasa shirika hilo ndio
shirika pekee la ndege hapa nchini linalotoa huduma zake kutoka Dar es Salaam
kuelekea visiwa vya Comoro na hivyo kutoa fursa kwa wananchi wa mataifa hayo
mawili kuweza kuunganisha fursa
mbalimbali zinazopatikana kwenye mataifa hayo ikiwemo biashara, kwa mujibu wa
Bw. Mfinanga.
Zaidi Bw. Mfinanga alibainisha
mpango wa shirika hilo wa kutambulisha safari zake za moja kwa moja baina ya
visiwa vya Comoro na Zanzibar kabla ya mwisho wa mwaka huu kutokana na uhitaji
mkubwa wa soko linachochewa na fursa za kibiashara baina ya visiwa hivyo.
Aliongeza kuwa pamoja na
mipango hiyo shirika hilo pia linaendelea kuboresha huduma zake kuelekea mkoani
Mtwara na limekuwa likijivunia kuwa kiungo muhimu katika usafiri kutoka Dar es
Salaam kuelekea mkoa huo ambao kwa sasa unajipanga kuchangamkia fursa ya uchumi
wa gesi iliyovumbuliwa hivi karibuni.
“Tumekuwa tukifanya safari
zetu kuelekea mkoani Mtwara kwa kipindi kirefu sasa. Fursa ya gesi iliyoibuka
mkoani humo inasababisha na sisi pia tujipange kwa kuangalia ni namna gani
tutanufaika na fursa hiyo pia. Lakini pia tuna jukumu la kuhakikisha tunatimiza
wajibu wetu kama shirika la taifa katika kukabiliana na mahitaji ya wananchi wa
taifa hili,’’ alisema.
Akizungumzia mipango ya
shirika hilo katika kujipanua zaidi, Bw. Mfinanga alisema kwa sasa shirika hilo
linaandaa mpango mkubwa wa miaka mitano ambao unatarajiwa kukamilika na kuwekwa
wazi hivi karibuni.
Kwa sasa shirika hilo
linatoa huduma zake kuelekea mikoa ya Kigoma, Mtwara na visiwa vya Comoro kwa
kutumia ndege yake aina ya CRJ-100
wakati ikiendelea kusubiri ndege yake nyingine aina ya De-Havilland Dash
8 Q300 inayoendelea na ukarabati mkubwa kwenye karakana ya shirika hilo iliyopo
kwenye uwanja wa Kimataaifa wa Julius Nyerere (JNIA) , jijini Dar es Salaam.
“Kukamilika kwa ukarabati
wa ndege hiyo kutasaidia tuweze kurejesha huduma zetu kuelekea mikoa ya Mwanza,
Tabora, Kilimanjaro na Mbeya,’’ alisema Bw Mfinanga.
ATCL: Utawala wa Rais Kikwete umetulindia hadhi yetu
Reviewed by crispaseve
on
05:33
Rating:
Post a Comment